Tanzania Kushiriki Mkutano wa Tathmini ya Usawa kwa Wanawake Duniani Maoni ya Pamoja: Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, na UN Women

UN Women

30/04/24

Descriptions

Mkutano wa Tume ya Hali ya Wanawake (Commission on the Status of
Women - CSW) unafanyika nchini Marekani Machi 11 hadi 22, 2024 ukiwa na lengo
la kutathmini maendeleo yaliyofikiwa katika usawa wa kijinsia duniani.



Mkutano huu wa 68 utashirikisha wawakilishi kutoka Serikalini, Mashirika
ya Kiraia na Mashirika ya Umoja wa Mataifa duniani kote.



CSW kwa kawaida hufanyika kila mwaka mjini New York nchini Marekani
ikiwa ni mkusanyiko mkubwa zaidi duniani wa haki za wanawake, ambapo wadau
wakuu hukutana pamoja ili kutathmini maendeleo ambayo yamepatikana katika
kufikia usawa wa kijinsia na kazi ambayo inahitajika kufanywa.



Kwa mara nyingine mwaka huu, ujumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ukiongozwa na wawakilishi wa Serikali kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar, wakiwa pamoja na wanachama wa Asasi za Kiraia, tutashiriki ili kusisitiza
tena ahadi mpya za kuongeza kasi ya kupatikana kwa usawa wa kijinsia.



Hii ni pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote, kwa
kuzingatia mada kuu ya mwaka huu: "Kuongeza kasi ya kufikia usawa wa
kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote kwa kushughulikia umaskini
na kuimarisha taasisi na kufadhili kwa mtazamo wa kijinsia."



Makadirio ya sasa yanaonyesha kwamba kama mwelekeo huu wa sasa
utaendelea, basi wanawake na wasichana milioni 342.4 kote duniani hawatakuwa
wameondoka kwenye umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030.



Hivyo CSW inatumika kama jukwaa muhimu kwa Tanzania kuonyesha
mafanikio yake katika kufikia ahadi za usawa wa kijinsia kimataifa na kitaifa
pamoja na kuangazia maeneo ambayo yanahitaji kuimarishwa zaidi, ikiwa ni pamoja
na kujifunza kutoka nchi nyingine duniani kote zinazoshiriki katika usawa.



Mfano mzuri ni nafasi ya nchi yetu kama kiongozi mwenza wa Muungano
wa Kimataifa wa Utekelezaji wa Jukwaa la Usawa wa Kizazi kuhusu Haki na Haki za
Kiuchumi, unaosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan, ambayo imeleta maendeleo makubwa.



Utekelezaji wa Mpango  wa
Kizazi chenye Usawa – Generation Equality Tanzania (2021/2022-2025/26) unalenga
kuimarisha huduma za umma na binafsi zinazozingatia jinsia, kuweka mazingira
wezeshi kwa kazi zenye staha za wanawake, kuboresha upatikanaji wa rasilimali
za wanawake, na kuendeleza sera za kiuchumi zinazozingatia jinsia, kwa
kushirikiana na sekta za umma na binafsi.



Katika CSW, tunatarajia kuangazia maendeleo makubwa chini ya
programu hii, ikijumuisha marekebisho ya sera ya kitaifa ya jinsia na
uimarishaji wa sheria, sera na mikakati inayozingatia jinsia.



Pia, upanuzi wa upatikanaji elimu na huduma za afya, kuongezeka kwa
ujumuishaji wa kifedha kwa wanawake, uwekezaji unaoendelea katika kuongeza
juhudi za kushughulikia kanuni hatari za kijamii zinazochochea ukatili dhidi ya
wanawake na wasichana.



Vilevile, hatua ambayo nchi inachukua ili kuimarisha ushiriki wa
wanawake, ikiwa ni pamoja na wanawake vijana na wanawake wenye ulemavu, katika
nafasi za uongozi na maamuzi.



Tanzania pia itaangazia maendeleo yake katika upangaji wa bajeti
unaozingatia jinsia, eneo muhimu ambalo Serikali kwa kushirikiana na UN Women
na wadau wengine, imejumuisha bajeti inayozingatia jinsia katika sekta
mbalimbali ikikihakikisha mifumo ya kiuchumi ya kitaifa inawawezesha wanawake
ipasavyo.



Kwa kushirikiana na UN Women, ESRF, WiLDAF, Landesa, LSF na LHRC,
Tanzania pia inaandaa matukio mawili ya pembeni kwenye mkutano huo wa CSW ili
kushirikishana mafanikio yaliyopatikana katika bajeti na ufadhili unaozingatia
jinsia, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa umma kwa mipango inayomilikiwa na
kuongozwa na wanawake.



Pia, utengaji wa fedha maalumu kwaajili ya wanawake na wasichana na
ukuzaji wa haki za ardhi za wanawake kupitia ‘Kampeni ya Simama kwa Ajili ya
Ardhi Yake’ (Stand for Her Land, S4HL).



Kwa kushiriki katika CSW 2024, Tanzania sio tu inathibitisha
kujitolea kwake katika kuendeleza usawa wa kijinsia lakini pia ina jukumu
muhimu katika kuunda ajenda ya kimataifa ya jinsia.



Tunajivunia ushirikiano mkubwa kati ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na UN Women, ambao umekuwa na mchango mkubwa
katika kuratibu ushirikishwaji wa Tanzania na kuongeza kasi ya juhudi za kutimiza
ahadi.



Ahadi ambazo ziliainishwa katika Lengo la 5 la Malengo ya Maendeleo
Endelevu ili kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana
wote.



Kupitia CSW na kwingineko, tumedhamiria kuendeleza kasi hii, yenye
kuleta mabadiliko na kukuza ulimwengu ambapo ushirikishwaji, ustawi, na
maendeleo endelevu ukiwa ni kwa wote.



 



 


Fanya Biashara yako ikue zaidi.

CATEGORIES

Apply For An Advert.


Email